The Youth voice column intends to describe a strategy in which young people are authentically engaged in working toward changing the systems that directly affect their lives.

Latest Posts:

WARAKA WA “SIRAJI” KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU TANZANIA

Image result for UNIVERSITY STUDENTS UDOM
Nitumaini langu kubwa kuwa ndugu zangu wanafunzi wa vyuo vikuu muwazima wa afya. Naomba nitoe pole kwenu wanachuo kwa kila yaliyowakuta wakati mkiwa safarini kuelekea kilele cha mafanikio. Naamini kuwa safari yenu ni ngumu kufika mnapopataka na ina vikwazo vingi sana ikiwa ni pamoja na usimamizi mbovu wa sera ya elimu ya juu pamoja na ubovu wa sera ya mkopo. Naamini kuwa pole yangu ni bora kuliko pongezi kwa maana ya kuwa “hakuna kheri inayopatikana bila shari nyuma yake!!!” Hivyo naamini kuwa “siku zote ili uweze kufikia kheri yoyote basi huna budi kupambana na shari iliyozunguuka kheri hiyo


Shari hiyo unayopambana nayo ndiyo inayokupa ujuzi (skills & experience) wa  kupambana na matatizo katika jamii yako. Shari hiyo ndiyo matokeo ya mafanikio yako ya baadaye. Shari hiyo ndiyo hugeuka na kuwa furaha baadaye hivyo tutambue kuwa “furaha yetu ya leo ni matokeo ya huzuni uliyopambana nayo jana”. Kusudio la waraka huu ni kujaribu kuibua mijadala wa kifikra katika akili zetu. Mijadala hiyo ndiyo chanzo cha kuleta mabadiliko chanya katika jamii zetu. Kwa kuwa ni mijadala ya kifikra hivyo katika kufikiri huko huwa naibua mawazo kwa kulinganisha na hali halisi huku nikiamini kuwa “truth is the conformity between intellect and reality”

Hivyo naomba bila pingamizi lolote lile, uniruhusu nizame katika fikra zako na nipandikize fikra hizi lakini kabla ya kukubali kuchukua mawazo yangu  kwanza na wewe jaribu kushughulisha akili yako katika kutafakari kila neno unalokutana nalo hapa, tena fanya tafakuri zito kwa maana pana huku ukihusianisha na hali halisi ya mazingira tunayoishi.

Elewa kuwa wakati wewe usomapo waraka huu, kuna wenzako wengi wanapenda kuwa kama wewe kwenye mazingira uliyonayo sasa lakini bila kujua kusudio la Mungu ambaye amekuchagua wewe ili akutumie kuwanufaisha wengine. Jiulize uko tayari kuitumikia jamii yako sasa? Uko tayari kuondoa huzuni uliyonayo sasa? Au uko tayari kuisaliti jamii yako kwa kujipandikiza mbinu za kifisadi ili kujinufaisha wewe peke yako?

Elewa kuwa kesho ni matokeo ya ulichofanya leo kwa kile ulichokiwaza jana. Tufahamu kuwa kufika kwetu kesho ni matokeo ya kile tunachokitengeneza leo na hiki tunachokitengeneza leo ni matokeo ya kile tulichokiwaza jana. Mwandishi mmoja aliwahi kuandika “…….life is experience, experiment, and expectation…….yesterday is experience, today is experiment and tomorrow is expectation”. Hivyo tuzingatie kuwa matarajio (expectation) yetu ya kesho hutokana na matendo (experiments) yetu ya leo ambayo kwayo tumefanya kutokana na ujuzi (experience) wetu wa jana.

Hapa nazungumizia juu ya kile tunachopata leo hapa chuoni ambacho ni elimu. Elimu hii ndiyo ujuzi wetu, maarifa yetu, na ndiyo ngao yetu. Elimu tuipatayo ndiyo silaha ya kupambana na shari iliyoko mbele yetu, ili tuweze kuipata furaha baada ya shari hiyo. Nasema hivi huku nikiamini kuwa shule (chuo) ndiyo maisha halisi kwa kuazima maneno ya mwanafalsafa mmoja anayesema “a school should not be a place for preparation of life, a school should be life

Image result for UNIVERSITY STUDENTS UDOMKwa kuongezea hapa Mwl. Nyerere katika hotuba yake ya “Education for self reliance and not for selfishness 5, March, 1998” Mwalimu alisemu  “……nobody is asking us to love other than we love ourselves, but those of us who have been lucky enough to receive a good education have a duty also to help to improve the well being of the community to which we belong it is part of loving ourselves” Kwa maana ya kuwa “…….hakuna mtu anayetulazimisha kupenda wengine zaidi ya kujipenda wenyewe lakini kwa wale waliobahatika kupata elimu nzuri wanawajibu wa kusaidia kuinua maisha ya jamii tutokazo, huko ndiko kujipenda wenyewe” (tafsiri ni yangu)

Hivyo kama sisi ni miongoni mwa wale waliobahatika kupata elimu je! Fikra zetu zimelenga kuinua maisha ya jamii tutokazo? Je! Ni kweli sisi tunajipenda wenyewe? Au sisi ni wabinafsi? Je! Mipango yako imelenga kutumia elimu uipatayo kama mwalimu alivyoelekeza? Je! Kuwa kwako hapa chuoni kuna umuhimu gani hasa kwa jamii utokayo? Ni nani hasa anapaswa kuleta maisha bora kwa wanakaya?

Hebu jaribu kufikiria maisha anaishi bibi na babu yako. Fikiria imani aliyonayo baba, mama na mlezi wako! Fikiria heshima uliyonayo mtaani kwenu ambayo kwayo umeipata tu baada ya kufika hapa Chuoni Angalia, tafakari na tambua jukumu lako juu ya umasikini unolitafuna taifa lako. Tambua na iheshimu nafasi yako kwa jamii. Ondoa mawazo mgando ya kuwa wewe ni taifa la kesho. Fahamu ya kuwa KESHO HUJENGWA NA LEO. Mchango wako kwa jamii ni upi? Mchango wa elimu yako kwa jamii ni upi? Ni zipi fadhila utatoa kwa jamii yako?

Fikiria juu ya familia yako inayotegemea kilimo cha mkono kwa zaidi ya miaka (50) hamsini huku wakisikia sera ya kilimo kwanza redioni tu. Jaribu kufanya tafakuri zito juu ya walezi wetu wanaopika chapati na vitumbua ili tu waweze kutusomesha. Je! Elimu unayopata hapa inamanufaa gani kwako na kwa jamii yako?

Nikitizama sura zenu, naona ishara ya hasira, machungu na huzuni iliyotanda mioyoni mwenu na manung’uniko yasiyoisha juu ya namna msivyoridhishwa na utendaji wa serikali yenu hasa kuhusu masuala yanayohusu elimu, mikopo huku wengine mkisoma waraka huu mkiwa mmeshika matumbo yenu na kuashiria NJAA kwani bado hata hamjapokea mkopo (boom) na hamjui ni lini mtapokea lakini yote na yote naomba kwa mbali muisikie sauti yangu ikisema “Ni dhahiri kuwa ubinafsi wetu tuna makuzi na malezi tofauti, tuna malengo na matarajio tofauti, tuna hulka na fursa tofauti. Lakini bayana kati ya yote hayo ni malengo linganifu ya kutaka kupata elimu. Elimu bora hupatikana kwa jitihada na uvumilivu, kujituma na kujieleza, kutafakari na kutafakuri. La muhimu ni kukaidi fikra hasi na tabia potofu na kukumbatia busara na uelewa” (Prof. Mlacha S, Quest for Knowledge Vol. 3, 2009:36)

Ni elimu na maarifa ndivyo vinaweza kutuondoa katika umasikini kwa kutubadili kutoka watafutaji wa kazi na  kuwa watengenezaji kazi, kutoka kuajiariwa hadi kujiajiri wenyewe. Ni elimu ndiyo itakayotupa uwezo wa kufikiri, kutafakari na kutafakuri tena kufanya tafakuri zito juu ya namna ya kuondokana na umasikini unaolitafuna taifa hili

Mwisho naomba nimalizie kwa kuazima maneno ya baba wa taifa kama alivyotafsiri maana halisi ya chuo kikuu. Mwalimu anasema “…Chuo kikuu ni taasisi ya elimu ya juu ambapo akili ya binadamu hufundishwa kufikiri kwa kina, kufikiri kwa uhuru na kuchambua pamoja na kutatua matatizo kwa hali ya juu kabisa”. Je! Elimu itolewayo vyuoni mwetu inamalengo haya? TAFAKARI

Ndugu, wanafunzi na wananchi naomba kuwasilisha.

Na Muhsin Siraji
0717664685
Share on Google Plus

About Muhsin Hero

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

INSTAGRAM @MUHSINHERO